TANZANIA YAIKARIBISHA AUSTRIA KUONGEZA UWEKEZAJI KUELEKEA DIRA YA 2050

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya (Mb), amekaribisha kuimarishwa kwa ushirikiano wa kina kati ya Tanzania na Austria, wenye lengo la kukuza biashara na uwekezaji endelevu kwa manufaa ya pande zote mbili kupitia fursa mbalimbali zilizopo chini ya Dira ya Maendeleo ya Taita 2050.

Dkt. Chaya ameyasema hayo tarehe 23 Machi 2026 jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Mhe. Balozi Dkt. Hannah Liko.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Chaya amewasilisha vipaumbele vya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kipato cha juu unaoongozwa na viwanda, wenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani trilioni 1.

Amebainisha sekta za kilimo, utalii, viwanda, madini pamoja na uchumi wa bluu zimeainishwa kuwa injini kuu za mageuzi ya kiuchumi.

Aidha, ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kujipambanua kama lango la soko la kikanda lenye zaidi ya watu milioni 450, hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutoka Austria.

Ameongeza kuwa ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia 6.1 kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita ni ishara ya uthabiti wa mazingira ya uwekezaji nchini.
Sambamba na hilo, amepongeza Mkakati wa Austria kwa Afrika unaolenga kukuza biashara na kuimarisha viwanda vidogo na vya kati (SMEs).

Comments