Waziri
wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha kuwa, hakuna mfanyabiashara anayeficha
mafuta kwa kisingizio cha kusubiri bei za mafuta zipande kutokana na mgogoro
unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati ambao umepelekea baadhi ya nchi
kukumbana na changamoto za upatikanaji wa mafuta.
Akizungumza jijini Dodoma katika kikao na Taasisi za Wizara zinazosimamia Sekta ya Mafuta, Mhe. Ndejembi ameeleza kuwa nchi ina usalama mkubwa wa mafuta na kwamba Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha wananchi katika maeneo yote wanapata huduma bila vikwazo hivyo EWURA anapaswa kuhakikisha hakuna mafuta yanayofichwa katika maghala ya kuhifadhi Mafuta.
Aidha,
ili kuhakikisha mafuta yote yaliyoagizwa nje ya nchi yanafika nchini kwa mujibu
wa mkataba, Mhe. Ndejembi ameelekeza kuundwa kwa timu maalum kufuatilia
mwenendo wa uingizaji wa Mafuta nchini ambayo itahusisha Wataalam kutoka Wakala
wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA),
EWURA, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Ulinzi
na Usalama.
" Timu hii itakuwa na jukumu la kufuatilia hatua kwa hatua na kuhakikisha kuwa mafuta yote yaliyoagizwa ambayo yako njiani kuja nchini yanafika kwa wakati bila kikwazo wala changamoto yoyote. Hali ya biashara ya mafuta huko duniani si ya kuridhisha, baadhi ya nchi bei ya mafuta imepanda maradufu na wafanyabiashara wengine wanaweza kuingia tamaa na kupeleka mafuta huko, katika hili sitarajii kuona mikataba tuliyoingia na waagizaji wa mafuta ikikiukwa." Amesisitiza Mhe. Ndejembi
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amewahakikishia Watanzania kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta hadi mwezi Julai 2026.
Amesema Serikali ilichukua hatua za mapema kwa kushirikiana na taasisi zake, ili kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta na kwa gharama himilivu.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kusimamia Taasisi zake ili kuhakikisha mafuta yaliyopo njiani yanafika kwa wakati, pamoja na kuwadhibiti wauzaji ili wasitumie changamoto iliyopo kama fursa ya kupandisha bei.
Awali,
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) Bw. Erasto
Simon alieleza kuwa hali ya upatikanaji wa mafuta nchini iko salama ambapo ameeleza kuwa ukijumuisha mafuta
yaliyopo nchini na yaliyopo njiani kuna petroli lita milioni 474 inayotosheleza
siku 78, dizeli lita milioni 392
inayotosheleza siku 50 pamoja na lita milioni 55 za mafuta ya ndege zinazotosheleza
siku 91.
Naye,
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw.Mussa
Makame ameeleza kuwa kuna mafuta ya kutosha ndani ya nchi na ambayo yako
safarini kwani Serikali ilishasaini mikataba na wazabuni mapema kwa ajili ya
uingizaji wa mafuta.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA,
Dkt. James Andilile ameeleza kuwa kwa sasa soko liko sawa hakuna mfumuko wa bei
hivyo EWURA itahakikisha watu hawafichi
mafuta kusubiri mfumuko wa bei katika soko la dunia.
Amesema EWURA imeendela kushirikiana na wadau wa mafuta wakiwemo waagizaji na wauzaji ili kuhakikisha kama kuna changamoto zozote zinatatuliwa kwa haraka ili wananchi wapate huduma kwa uhakika.





Comments
Post a Comment