DKT. FATMA MGANGA ATOA SOMO ZITO AKIFUNGUA KIKAO KAZI CHA TARURA MKOA WA SINGIDA

 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka watumishi wa TARURA kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuhakikisha barabara zinapitika na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Akizungumza katika kikao kazi cha TARURA kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Ukaguzi Mkoa wa Singida, Dkt. Mganga amesema TARURA ni taasisi mtambuka inayochochea maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na uchumi.


Amesisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuwa na mawasiliano mazuri na kuwahudumia wananchi kwa heshima kuwakumbusha watumishi kupambana na vitendo vya rushwa, kuheshimu muda wa kazi na kujaza taarifa katika mfumo wa PEPMIS.

Aidha, amewahimiza watumishi kutunza afya zao kwa kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara na kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi, akieleza kuwa afya ya mtumishi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Taifa.


Awali, Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Claver Mwinuka, amesema kikao kazi hicho kinalenga kujadili mipango ya kazi, bajeti ya mwaka ujao wa fedha pamoja na mikakati mipya ya utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia maelekezo ya Bodi ya Barabara.


Ameongeza kuwa kikao hicho pia kitatoa fursa ya kuimarisha mahusiano na mawasiliano kati ya watumishi, wengi wao wakiwa wapya, pamoja na kujadili matumizi ya teknolojia ya mawe katika ujenzi wa barabara ili kupunguza gharama na kuboresha ubora wa miundombinu.

Comments