Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu makadirio na matumizi ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.
Ametoa agizo hilo leo Jumanne (Machi 10, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Kasanga, Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, ambapo baadhi ya majengo bado hayajakamilika licha ya fedha kutolewa na Serikali.
Serikali ilitoa zaidi ya Sh. bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kalambo ambapo katika awamu ya kwanza majengo saba ya huduma za afya yalijengwa, ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mama na mtoto, maabara, duka la dawa pamoja na miundombinu mingine ya huduma za hospitali. Hata hivyo, licha ya fedha hizo kutolewa na baadhi ya majengo kukamilika, majengo mawili muhimu ambayo ni jengo la theatre (chumba cha upasuaji) na wodi ya wanaume hayajakamilika.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu ameonesha kutoridhishwa na taarifa ya kuchelewa kukamilika kwa baadhi ya majengo ya hospitali hiyo.
“Ninyi mmeomba fedha, hamjapunguziwa hata senti moja ya fedha mlizoomba, mmepewa. Halafu mnapofika kwenye utekelezaji mnasema fedha haitoshi. Hii si sawa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Mwigulu amemtaka Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Rukwa Bw. Mzalendo Widege kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kulikuwa na uzembe au udanganyifu katika makadirio na matumizi ya fedha za ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ili kuboresha huduma za matibabu nchini.
Amesema katika kipindi cha takribani miaka minne, Serikali imejenga vituo vya afya zaidi ya 649 na zahanati zaidi ya 2,800 ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Aidha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amewataka watendaji wote wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha wanashughulikia migogoro ya ardhi kwa uadilifu na weledi ili kuondoa malalamiko ya wananchi yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kuwa katika maeneo mengi aliyopita, migogoro ya ardhi imeonekana kuwa miongoni mwa kero kubwa zinazowakabili wananchi huku ikichangia zaidi ya asilimia 90 ya malalamiko yanayowasilishwa katika mikutano ya hadhara.
Awali, Dkt. Mwigulu alikagua miundombinu na utendaji kazi wa Bandari ya Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Akimpa taarifa ya maboresho hayo, Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA Erick Madinda alisema kuwa Bandari ya Kasanga ilijengwa kuanzia Aprili 29, 2019 hadi Aprili 28, 2020 kwa gharama ya takribani Sh. bilioni 4.7. Miundombinu iliyopo bandarini hapo ni pamoja na gati la kuegesha vyombo vya majini lenye urefu wa mita 120 na kina cha mita 14, jengo la kusubiria abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 200 kwa wakati mmoja pamoja na maghala mawili ya kuhifadhi mizigo yenye uwezo wa tani 2,500 kila moja.
Taarifa ya utendaji inaonesha kuwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Desemba 2025, bandari hiyo imehudumia jumla ya tani 3,418 za mizigo, abiria 3,648, meli 11 pamoja na maboti 337. Miongoni mwa mizigo inayohudumiwa katika bandari hiyo ni saruji, makaa ya mawe pamoja na mazao ya chakula kama mahindi, mchele na unga wa sembe.
Comments
Post a Comment